Wednesday, August 28, 2013

Watu milioni mbili nchini wakadiriwa kuwa wana ugonjwa wa kichocho






Na Elizabeth Joseph,Dodoma.
IMEELEZWA  kuwa jumla ya watu Milioni Mbili wamebainika kuwa na ugonjwa wa Kichocho Nchini.
Hayo yalielezwa juzi na Daktari Kitengo cha Kichocho na Matende Dk.Phenehas Machumu katika Manispaa ya Dodoma wakati akitoa elimu juu ya ugonjwa huo katika kikao cha Wazazi kilichofanyika katika Shule ya Msingi Amani iliyoko Manispaa ya Dodoma Mjini kilicholenga kujadili Utoaji wa dawa za ugonjwa huo kwa watoto walioko shule.
Machumu alisema kuwa kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa na wanasayansi  imebainika kuwa idadi ya watu waliokutwa na tatizo hilo ni Milioni Mbili Nchini ambapo kwa Dunia nzima ni  Milioni tano na kuongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga kutokomeza ugonjwa huo.
Aidha aliwataka wananchi kuwa wepesi wa kupima afya zao katika magonjwa yote ili kujua kama wana maambukizi ya ugonjwa huo kwakuwa unaweza kuonekana kwa muda wa miaka kadhaa hali inayosababisha wengine kupoteza maisha bilakujua kama wana tatizo hilo.
Machumu pia alibainisha kuwa kwa Mkoa wa Dodoma mzunguko wa ugonjwa huo umefika asilimia 30 jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama wa wakazi wake hivyo kuwaomba wananchi kuungana na Wizara ya Afya katika kutoa elimu juu kutokomeza tatizo hilo na hatimaye kupunguza asilimia hiyo.
Pia aliwataka wazazi kujiandaa kisaikolojia kwa kukubali watoto wao kupewa dawa ya ugonjwa huo ili kutibu na kukinga maambukizi ya tatizo hilo kwakuwa katika kikao hicho wazazi wengi  walionekana kuingiwa na hofu juu ya dawa hizo kwa kuhofia madhara yanayoweza kujitokeza mara baada ya mtoto kupewa dawa hizo kwakuwa mwaka 2011 wakati wa utoaji dawa hizo baadhi ya wanafunzi katika shule kadhaa walianguka kwa kizunguzungu,kichefuchefu na usingizi.
Kampeni dhidi ya Kichocho Kitaifa ilianza mwaka 2011 kwa kuwapa dawa za kinga watoto walioko Shule za Msingi wenye umri wa miaka mitano hadi kumi na nne kwakuwa imebainika kuwa wao ndio wako katika hatari zaidi ya kupata ugonjwa huo kutokana na mazingira wanayokutana nayo ambapo kwa Manispaa ya Dodoma zoezi la ugawaji wa dawa hizo litafanywa Agosti 30 Mwaka huu katika Shule zote za Msingi.

No comments:

Post a Comment