Thursday, August 29, 2013
SPIKA MAKINDA AINGIA KATIKA ORODHA YA WANAOTARAJIA KUWANIA URAIS
Na Bilson Vedastus - Dodoma
Harakati za kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimeanza kuchukua sura mpya, baada ya baadhi ya vigogo kujitokeza hadharani kumpigia debe Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Vigogo hao ambao wana ushawishi ndani ya CCM walishindwa kujizuia na kulazimika kumpigia debe Makinda ndani ya ukumbi wa Bunge jana, huku wakimwagia sifa za kuwa Rais wa Tanzania baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake kwa mujibu wa kikatiba.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Anna Abdallah, alimmwagia sifa spika huyo kuwa anafaa kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mbunge huyo ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT) na waziri kwenye serikali ya awamu ya pili na ya tatu , alitoa kauli hiyo alipokuwa akiunga mkono hoja ya Mwenyekiti wa Chama cha Mabunge ya Afrika (CPA) tawi la Tanzania Mussa Azzan Zungu, kumpongeza Spika Makinda kwa kuteuliwa kuwa Rais wa chama hicho Afrika.
Anna Abdallah, ambaye pia aliwahi kushika wadhifa wa ukuu wa mkoa katika utawala wa awamu ya kwanza, alisema uteuzi wa Spika Makinda, siyo heshima kwake tu bali ni kwa Watanzania wote, lakini hasa kwa wanawake.
Alisema haoni sababu ya kwa nini Spika Makinda sasa asigombee CPA ngazi ya kimataifa kwani yeye pamoja na Watanzania na wabunge kwa ujumla watamuunga mkono.
Alisema kwa msingi huo, anamshauri Spika Makinda kutokana na kuwa na uzoefu wa kutosha ndani na nje ya nchi kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Kwa upande Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Profesa Mark Mwandosya, wa Rungwe Mashariki, alisema Spika Makinda amekuwa mfano mzuri wa kuigwa kutokana na uongozi wake tangu akiwa mkuu wa mkoa, mbunge, naibu waziri, waziri kamili, naibu spika na sasa spika.
Profesa Mwandosya ambaye pia ni Mbunge wa Rungwe Mashariki akiwa amejitosa kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2005 na kuishia kwenye nafasi ya tatu bora kabla ya yeye na Dk. Salim Ahmed Salim kubwagwa na Rais Jakaya Kikwete kwenye mkutano mkuu wa CCM, alimwelezea Spika Makinda kuwa ni mtu mwadilifu, mtenda haki, anayejiamini, mvulimivu, mnyenyekevu, msikivu na mwenye msimamo, hivyo hashangai kupitia yeye (Spika), Bunge lijalo hata bila ya Katiba mpya, wanawake watafikia asilimia 55 katika Bunge.
Profesa Mwandosya alisema hiyo inatokana na ukweli wa historia yake ya uongozi wasichana wengi sasa wanataka kuwa viongozi, lakini pia wanawake wengi watajitokeza kugombea ubunge.
Hata hivyo, Profesa Mwandosya hakutaja moja kwa moja kama Spika Makinda anapaswa kugombea urais mwaka 2015, isipokuwa alisema kwa wale wanaofikiria 2015 watambue kwamba (Makinda) ni tishio kwao.
Kupigiwa debe kwa Makinda kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kunaongeza idadi ya makada wa CCM wanotajwa kuwania uteuzi wa chama hicho tawala.
Hadi sasa wanaotajwa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta; Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment