Friday, August 30, 2013
Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia amewataka watendaji wa wizara yake wanaoshiriki katika mitandao ya kubeba wabadhirifu ndani ya ofisi hiyo kujipima na kujiondoa wenyewe.
Na.Bilson Vedastus, Dodoma
Ghasia amebainisha hayo wakati wa hafla fupi katika kuwakaribisha watendaji wa wizara hiyo iliyofanyika mjini Dodoma.
Amesema hivi sasa ndani ya Tamisemi kuna mitandao ya kulea wabadhirifu na kumtaka kila mtu kujipima mahali alipo ili kuondoa kasoro hizo.
“Sasa nataka nisema kuwa kwa mtumishi au mtendaji ambaye hatakwenda na sisi tutahesabu kosa na hatutabembeleza mtu , tunataka kila mtu atimize wajibu wake katika eneo lake na hapa sitamwonea mtu na hatupo tayari kumbeba mtu.” alisema.
Alisema kwa muda mrefu amefanya kazi na timu ambayo ilikuwa haijakamilika jambo ambalo lilimfanya kufumbia macho baadhi ya mambo.
Alisema kukamilika kwa uteuzi wa Katibu Mkuu na manaibu makatibu wakuu wa wizara hiyo, kunaifanya timu kukamilika.
Lakini pia aliwataka makatibu wakuu hao waliopewa dhamana na Rais kusimamia sekta mbalimbali ndani ya wizara hiyo kuacha kujifungia maofisini na badala yake watoke na kwenda mikoani na wilayani kufuatilia kero za wananchi na kuzipatia ikiwa ni sambamba na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu mpya wa Tamisemi, Jummane Sagine, alikiri kuwapo kwa mitandano hiyo ya ubadhilifu ndani ya wizara hiyo.
“Kweli vitendo hivi vya mitandao na hata ubadhirifu niliviona kwa macho yangu na wakati mwingine niliambiwa lakini nilikuwa mpole katika kipindi hicho cha kukaimu,” alisema.
Aliwaonya baadhi ya watendaji wanaofanya ubadhirifu kwa ajili ya tamaa ya fedha kuacha.
Vilevile Katibu aliwaonya watendaji ndani ya wizara hiyo kuachana na porojo za siasa ndani ya ofisi hiyo ambayo ni muhimu kwa jamii.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment