Friday, August 30, 2013

"Si ajabu yaani kwa CCM tu, mbona nanyi chama chenu kilifanya hivyo ingawa mbunge wenu bado ni mbunge?,"

  
 








MZIMU wa kutimuliwa kwa aliyekuwa Mwakilishi wa Kiembesamaki, Mansour Yussuf Himid (CCM), umeibukia bungeni baada ya Mbunge wa Micheweni, Haji Khatib Kai (CUF), kudai kuwa kufukuzwa kwake ni kinyume cha Katiba ya nchi. Kai, aliseyasema hayo jana alipokuwa akiuliza swali kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambapo alisema Ibara ya 18 ya Katiba imetoa uhuru kwa mwananchi yeyote kujieleza ili mradi havunji sheria.

Kabla ya kujibu swali hilo, Pinda alimtaka mbunge huyo kutaja jina la kiongozi anayemzungumzi, ndipo mbunge huyo alipomtaja Mansour na kuwafanya wabunge kuangua kicheko.
Pinda alilijibu kwa kifupi huku akimrushia kijembe mbunge huyo kwa kusema kwamba si jambo la ajabu mwakilishi huyo kufukuzwa mbona chama cha CUF kilimtimua mbunge wao.
"Si ajabu yaani kwa CCM tu, mbona nanyi chama chenu kilifanya hivyo ingawa mbunge wenu bado ni mbunge?," alihoji Pinda kwa kifupi.
Agosti 26, mwaka huu Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) ilitangaza kuridhia kuvuliwa uanachama kwa Mansour kama ilivyopendekezwa na Halmashauri Kuu ya chama hicho Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar.
Hatua hiyo, ilitokana na mjumbe huyo kukabiliwa na tuhuma akidaiwa kushindwa kusimamia malengo ya CCM na kutekeleza masharti ya uanachama. Mengine kushindwa kutekeleza wajibu wa mwanachama na kukiuka maadili ya CCM na Ilani ya CCM ya mwaka 2010-2015.
Agosti 18, mwaka huu Kamati ya maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar, ilipitisha mapendekezo ya kumvua uanachama mwakilishi huyo na waziri wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.




No comments:

Post a Comment